Dhamira ya vidio ya 'Fitna' yalaaniwa na jamii ya kimataifa

Dhamira ya vidio ya 'Fitna' yalaaniwa na jamii ya kimataifa

Mataifa wanachama pamoja na KM wa Umoja wa Nchi za Kiislam yakijumuika vile vile Mataifa ya Ulaya wamelaani kipamoja vikali ile vidio iliotengenezwa na Geert Wilders, mwanabunge wa Uholanzi ambayo walisisitiza ilijaa \'kufuru\' dhidi ya WaIslam, na pia ilionesha chuki kwa wageni, na wanakhofia huenda ikasababisha utovu wa ustahamilivu wa kidini ulimwenguni. Kadhalika wanaamini dhamira hasa ya vidio hiyo, iliopewa jina la \'Fitna\' na iliosambazwa kwenye mtandao tangu wiki iliopita ilikuwa ni kuchochea chuki na vurugu miongoni mwa wafuasi wa dini.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour kwenye taarifa yake kuhusu vidio hiyo ya kashfa aliunga mkono shtumu za KM Ban Ki-moon pamoja na zile za Wakariri Maalumu wa haki za binadamu ambao walihisi lengo hakika, na maudhui ya uchokozi ya vidio ya Geertz, ilikuwa ni kuchochea hisia karaha kwa wafuasi wa KiIslam. Kwa mujibu wa Arbour kanuni za kimataifa zimejaaliwa mfumo wa hifadhi za kisheria ambazo angelipendelea kuona wafuasi waliokashifiwa wanazitumia kukhitimisha mzozo huo - na aliwahimiza wanasheria wa kimataifa kutekeleza majukumu yao kuhusu suala la vidio chini ya Vifungu vya 19 na 20 vya Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Kisiasa na Kiraia na kulinda uhuru wa makundi kutoa mawazo na kujieleza lakini bila ya kudhuru na kuteteta chuki dhidi ya kabila, taifa wala dini.