Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UM kuanzisha tena duru mpya ya mazungumzo ya Sahara ya Magharibi

Duru nyengine ya mazungumzo ya kutafuta suluhu juu ya mzozo wa Sahara ya Magharibi inatarajiwa kukutana katika mji wa Manhasset, kwenye Jimbo la Long Island, New York kuanzia Januari 7 hadi 9, majadiliano ambayo yatasimamiwa na UM. Kikao cha safari hii kitafuata taratibu ya mikutano iliopita, kwa kulingana na hisia kuu ya wawakilishi wa Morocco na Chama cha Ukombozi cha Frente Polisario, ambao hupendelea mazungumzo yao yawe ya faragha.

Operesheni za UNAMID katika Darfur zahitajia msaada ziada kidharura, asisitiza KM

Ripoti ya KM juu ya suala la kupeleka vikosi mseto vya UNAMID vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika Darfur imeonya kwamba mafanikio yaliojiri kwa sasa ni haba sana, na hayataviwezesha vikosi hivyo vya kimataifa kuyatekeleza majukumu yake kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama. Hali hii, alitilia mkazo, itaunyima umma wa Darfur utulivu na amani ya wa muda mrefu inayotakikana kidharura katika eneo lao.

Vurugu lazuka upya Cote d'Ivoire

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Cote d’Ivoire (UNOCI) limeshtumu hali ya kuzuka tena kwa vurugu karibuni kwenye eneo la Bouake, kaskazini ya nchi. Kwa mujibu wa taarifa ya UNOCI raia wasio hatia walikamatwa, na baadhi yao waliuawa kihorera, vitendo ambavyo UM umesisitiza vinakiuka kihakika haki za binadamu. Wenye madaraka walihimizwa kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha jinai hii inakomeshwa haraka, uhalifu ambao UNOCI unaamini unahatarisha usalama na amani ya taifa kijumla.

Tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya UM zapungua 2007 Liberia

Ripoti ya karibuni ya Shirika la UM juu ya ulinzi wa amani katika Liberia (UNMIL) imethibitisha kwamba shtumu dhidi ya wafanyakazi wa UM, ambao siku za nyuma walidaiwa kuendeleza ukandamizaji na tuhumu za unyanyasaji wa kijinsia, zimeteremka kwa asilimia 80 katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka 2007, tukilinganisha na kipindi hicho hicho katika 2006.