Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mbadala wa kuwa na mataifa mawili Mashariki ya Kati:Guterres

Hakuna mbadala wa kuwa na mataifa mawili Mashariki ya Kati:Guterres

Pakua

"Nitafanya kila niwezalo ndani ya uwezo wangu kuunga mkono viongozi wa Israel na Palestina kurejea katika meza ya majadiliano na kutambua mtazamo wa kuwa na amani ya kudumu kwa watu wa pande zote mbili."

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya umoja huo mjini New York Marekani kuhusu hatua za mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.

Guterres ambaye amesema anapinga hatua zozote zinakazoweka njia panda matarajio ya amani ya Israel na Palestina amesisitiza kuwa

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Yerusalemu ni suala la mwisho ambalo linapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili kwa kufuata msingi wa maazimio ya baraza la usalama na baraza kuu wakizingatia masuala ya muhimu kwa pande zote, Palestina na Israel”

Ameongeza kuwa anatambua hisia na umuhimu mkubwa wa mji wa Yerusalem katika nyoyo za watu wengi na imekuwa hivyo kwa karne na karne na itaendelea kuwa hivyo lakini ameongeza

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Katika wakati huu wa wasiwasi mkubwa, nataka kuweka bayana: hakuna njia mbadala ya ufumbuzi wa kuwa na mataifa mawili. Hakuna Mpango  wa pili.”

Amesisitiza kuwa hadi pale mtazamo huo wa kuwa na mataifa mawili yatakayoishi kwa pamoja kwa amani, usalama na kutambuana, na mji wa Yerusalemu kuwa mji mkuu wa Israel na Palestina na pia masuala yote kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya majadiliano ndipo matarajio ya kweli ya watu wa pande zote yatakapotimia.

Photo Credit
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala la mustakhbali wa amani Mashariki ya Kati hususan mji wa Yerusalem. (Picha:UN/Mark Garten)