Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Zanzibar na harakati za kulinda mazingira ili kuchangia utalii

Huko visiwani Zanzibar nchini Tanzania, uharibifu wa mazingira hususan maeneo ya baharini unatishia mustakhbali wa utalii ambao ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato visiwani humo. Katika mkutano wa hivi karibuni wa tume ya Umoja wa Mataifa kwa uchumi wa Afrika, ECA huko Comoro ambako washiriki kutoka serikali walipazia fursa na vikwazo vya uchumi. Miongoni mwao ni Aboud Jumbe ambaye ni mkuu wa utafiti na mipango, Idara ya Mazingira kwenye wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Haki ya tiba yaongeza wanaopata dawa kupunguza makali ya VVU-Ripoti

Kuelekea siku ya Ukimwi duniani tarehe mosi mwezi ujao, imeelezwa kuwa takribani watu milioni 21 hivi sasa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU wanapatiwa matibabu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya Ukimwi, UNAIDS limesema hay oleo katika ripoti yake mpya ikisema idadi hiyo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na watu 685,000 mwaka 2000.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé, amesema siri ya mafanikio ni ujasiri wa watu wanaoishi na VVU kudai haki yao ya msingi ya matibabu, sambamba na uongozi thatbiti na ufadhili wa kifedha.

Picha:WFP

WFP yapokea dola milioni 5 toka HNA, kusaidia wakimbizi Syria

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP leo  limetangaza kupokea dola milioni 5 kutoka shirika la misaada ya kibinadamu la China HNA ili kuwasaidia wakimbizi wa Syiria walioko  Uturuki,  na Lebanon kwa miaka mitatu ijayo  katika ubia mpya.

Ushirikiano huu kati ya WFP na HNA ulitiwa saini baina ya Mkurungezi mkuu wa WFP David Beasley na makamu mwenyeki wa HNA Li Xianhua mjini Beinjing China.

Mexico komesheni ubaguzi dhidi ya watu wa asili:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wa asili Tauli-Corpuz ameitaka serikali ya Mexico kuhakikisha inafikia uhusiano wenye usawa na heshima na watu wa asili ili kukomesha hali inayoendelea ya ukiukwaji wa haki za binadamu za watu wa asili.

Amesema anatambua na kupongeza hatua za kimataifa za kuiweka ajenda ya haki za watu wa asili katika jukwaa la kimataifa ikiwemo kuunga mkono kazi yake , hata hivyo amesema jukumu hilo lazima litekelezwe na serikali ya Mexicokwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Maendeleo ya viwanda Afrika yaende sanjari na ajenda 2030: Guterres

Uwekezaji madhubuti katika miundombinu baina ya nchi utasaidia kuboresha biashara na kuinua uwezo wa viwanda barani Afrika.

Hilyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kuhusu siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka Novemba 20.

Ameongeza kuwa kuchagiza teknolojia zinazojali mazingira na kutumia kiwango kidogo cha hewa ukaa vitatoa fursa ya kuongeza biashara na ukuaji wa viwanda.

WHO yalaani daktari wake kutekwa huko Libya, yataka aachiliwe haraka

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limethibitisha kutekwa kwa daktari wake mmoja kutoka kituo cha afya cha Sabha kilichoko mji wa Sabha kusini mwa Libya.

Kufuatia ripoti hizo, WHO imelaani vikali kitendo hicho ikitaka wahusika wa utekaji nyara wahakikishe usalama wake na aachiliwe huru mara moja.

Katika taarifa yake WHO imesema utekaji nyara wahudumu wa afya na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya ni kinyume na maadili na sheria na hukwamisha fursa za watu kupata huduma ya afya.

Hatima ya watoto milioni 180 mbaya kuliko wazazi wao: UNICEF

Licha ya hatua zilizopigwa kimataifa, mtoto 1 kati ya 12 duniani wanaishi katika nchi ambazo matarajio yao leo ni mabaya kuliko ya wazazi wao, kwa mujibu wa tathimini iliyofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya watoto duniani yanayofanyika leo.

Tathimini hiyo inasema watoto milioni 180 wanaishi katika nchi 37 ambako wana hatihati kubwa ya kuishi katika ufukara, kutosoma au kuuawa kikatili kuliko watoto walioishi katika nchi hizo hizo miaka 20 iliyopita.

Viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya Afrika:UNIDO

Leo ni siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika, kauli mbiu ikiwa “Maendeleo ya viwanda Afrika ni moja ya sharti la kuwa na eneo huru la biashara yenye ufanisi na endelevu (CFTA)”.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO  lengo la siku ya mwaka huu ni kuchagiza umuhimu wa maendeleo ya viwanda Afrika katika utekelezaji wenye mafanikio ya kuwa na eneo la biashara huru na hivyo kusaidia kukuza zaidi uchumi wa bara hilo na kupiga jeki harakati za kutokomeza umasikini.

Vyoo vinaokoa maisha, kinyesicho chenda wapi?:UM

Vyoo vinaokoa maisha kwa sababu kinyesi cha binadamu husambaza magonjwa yanayokatili maisha ya watu wengi. Leo ikiwa ni siku ya choo duniani Umoja wa mataifa unasema watu bilioni 4.5 wanaishi bila vyoo vya kuhifadhi uchafu wao, hivyo sikuu hii ni ya kuhamasisha kuchukua hatua ili kukabiliana na tatizo la usafi duniani.

Kwa mara ya tatu baraza la usalama lashindwa kuongeza muda wa JIM:

Kwa mara ya tatu ndani ya siku mbili baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa limeshindwa kupitisha azimio la jukumu la jopo la kimataifa linalochunguza matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria kutokana kwa sababu ya kura ya turufu ya Urusi nchi ambayo ni mjumbe wa kudumu wa baraza hilo.

Jukumu la shirika la pamoja la kupinga matumizi ya silaha za kemikali (OPCW)-na jopo la Umoja la Umoja wa Mataifa la mkakati wa pamoja wa uchunguzi (JIM) linamaliza muda wake hii leo.