Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyoo vinaokoa maisha, kinyesicho chenda wapi?:UM

Vyoo vinaokoa maisha, kinyesicho chenda wapi?:UM

Pakua

Vyoo vinaokoa maisha kwa sababu kinyesi cha binadamu husambaza magonjwa yanayokatili maisha ya watu wengi. Leo ikiwa ni siku ya choo duniani Umoja wa mataifa unasema watu bilioni 4.5 wanaishi bila vyoo vya kuhifadhi uchafu wao, hivyo sikuu hii ni ya kuhamasisha kuchukua hatua ili kukabiliana na tatizo la usafi duniani.

Kauli mbiu ya mwaka huu inahoji “kinyesi hicho chenda wapi? Umoja wa Mataifa unasema lengo ni kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu hususan lengo namba sita #SDG6 lihusulo maji safi na usafi linafikiwa na kupunguza kwa nusu kiwango cha maji taka , huku ikipandisha kiwango cha kusafisha maji hayo na kuyatumia tena.

Lakini ili lengo hilo litime umoja huo umesisitiza kinyesi cha kila mtu lazima kidhibitiwe, kisafirishwe, kisafishwe na kutupwa katika njia salama na endelevu.

Shirika la afya ulimwenguni WHO linasema leo hii mabilioni ya watu duniani mifumo yao ya usafi ama haipo au haifanyi kazi na hivyo kutoa tisho kubwa kwa afya na maisha ya watoto na binadamu wengine.

Pia mfumo duni wa maji na usafi unazigharimu nchi zinazoendelea takribani dola bilioni 260 kwa mwaka sawa na asilimia 1.5 ya pato lao la taifa.

Photo Credit
Watoto wa shule wakienda kujihifadhi chooni katika jitihada za kudumisha usafi. Picha na UM