Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Changamoto zinazowakabili wajane na juhudi za usaidizi Tanzania

Siku ya kimataifa ya wajane ambayo huadhimishiwa kila Juni 23, mwaka huu imejikita katika kuhakikisha ustawi wa kundi hilo ambalo mara kadhaa hukumbana na mateso katika jamii.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuna takribani wajane milioni 259 duniani kote na karibu nusu wanaishi katika hali ya umasikini. Umoja wa Mataifa unatetea haki za kundi hilo linalonyanyapaliwa na familia zao na jamii huku wengine wakikumbwa na ubaguzi sababu ya umri na jinsia.

WHO yalaani uharibifu dhidi ya vituo vya afya Libya

 

Shirika la afya ulimwenguni WHO limelaani mashambulizi ya hivi karibuni katika vituo viwili vya afya mjini Benghazi nchini Libya ambayo yameelezwa kusababisha uharibifu kwa majengo na vifaa tiba.

Taarifa ya WHO inasema kuwa mnamo Juni 21 roketi ilipiga paa lililokarabatiwa mwaka 2014 baada ya shambulizi wakati wa machafuko mwaka 2011.

Utesaji unaendelea kuenea licha ya kupigwa marufuku: Ban

Vitendo vya  utesaji  ambavyo ni kinyume na utu vinaendelea kuenea na inasikitisha kwamba vinaendelea kukubalika amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Ameyasema hayo katika tamko lake la kuadhimisha siku ya kimataifa ya usaidizi kwa wahanga wa uteswaji inayoadhimisha kila Juni 26.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa utesaji ni marufuku.

Ban amesema sheria dhidi ya utesaji iko wazi na kuongeza kuwa vitendo hivyo haivafai kutumiwa wakati wowote na katika hali zozote ikiwamo wakati wa machafuko au usalama wa taifa unapokuwa katika kitisho.

Pande kinzani Yemen zina wajibu wa kimaadili na kisiasa.

Pande kinzani katika mgogoro wa Yemen zina wajibu wa kimaadili na kisiasa katika kusitisha machafuko amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon jumapili.

Akiongea nchini Kuwait ambapo majadiliano ya upatanishi yamekuwa yakifanyika Ban ameelezea kusikitishwa kwake na hali tete katika eneo la mapigano.

Katibu Mkuu ambaye pia amekutana na mamlaka za mataifa ya Uajemi na kuwashukuru kwa usaudizi wao katika mchakato wa kusaka amani nchini Yemen, pia amezionya pande kinzani kuwa hakuna muda wa kupoteza.

Ban ahuzunishwa na mapigano Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea kusikitishwa kwake kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan SPLA na vikundi vyenye silaha mjini Wau,  na maeneo jirani  nchini Sudan Kusini.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imemnukuu akisema kuwa amesikitishwa na taarifa za vifo kufuatia machafuko hayo.

Amevitaka vikosi kinzani kusitisha uhasama hima, kuruhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS kufika katika maeneo hayo na kushirikiana na wadau wa misaada ya kibinadamu ili kuwezesha ufikishwaji wa misaada.

Jumuiya ya Ulaya chondechonde wathaminini wakimbizi,wahamiaji: Ban

Akiwa ziarani nchini Ufaransa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesisisitiza kuwa uamuzi wa Uingereza kujitoa katika jumuiya ya Ulaya EU, haupasiwi kuwa mzigo kwa wakimbizi, wahamiaji na wasaka hifadhi barani humo.

Akizungumza na vyombo vya habari akiwa ameambatana na mwenyeji wake Rais Francois Hollande, Ban amesema anatarajia nchi za Ulaya zitaheshimu sheria za  kimataifa na kuonyesha ubinadamu kwa makundi hayo yasiyo na hatia.

Umuhimu wa mabaharia utambuliwe : IOM

Baharini kwa wote ni kauli mbiu inayotumika kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya mabaharia leo Juni 25, 2016.

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, linaadhimisha siku hii kwa mara ya sita kwa kuangazia umuhimu wa mabaharia katika bahari duniani ambapo Katibu Mkuu wa IOM Kitack Lim amekaririwa akisema mabaharia hawatambuliwi huku wakitimiza jukumu muhimu la kuisongesha dunia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wa kuadhimisha siku hii amesema mabaharia wanalisha dunia, huvalisha na kuihifadhi.

Washindi wa tuzo ya UNFPA mwaka 2016 watuzwa

Wiki hii, mnamo Alhamis Juni 23, imefanyika hafla maalum kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ya kutoa tuzo ya Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu (UNFPA) kwa washindi wa mwaka 2016.

Tuzo hiyo ya kila mwaka hutolewa kwa mtu binafsi na shirika au taasisi inayojikita katika kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake, pamoja na afya ya akina mama na wajawazito.

Washindi wa mwaka huu wamebainishwa kwenye hafla iliyoghubikwa kwa muziki na shangwe. Kujua washindi hao ni akina nani, ungana na Assumpta Massoi katika makala hii.

Harakati za kulinda watu wenye ualbino

Kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 17 mwezi Julai mwaka 2016 nchini Tanzania, kulifanyika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu harakati za kulinda watu wenye ulemavu wa ngozi , au ualbino. Lengo la mkutano huo wa kwanza kabisa katika kanda ya Afrika lilikuwa kuleta pamoja viongozi wa serikali, mashirika ya kiraia na watu wenye ualbino ili hatimaye kuibuka na mipango inayotekelezeka mashinani. Je nini kilijiri?

(Makala)

Mafanikio ya Somalia katika masuala ya haki yamulikwa Geneva

Baraza la Haki za Binadamu limekutana leo kwa ajili ya kuzungumzia tathmini ya mara kwa mara ya Somalia, nchi wanachama zikipongeza nchi hiyo kwa jitihada katika kuendeleza haki za wanawake.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kwamba nchi wanachama zilizohudhuria mkutano huo zimemulika mafanikio yaliyopatikana nchini Somalia katika kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu, uwezeshaji wa wanawake na haki za watoto.