Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Neno La Wiki

Neno la wiki: Hiba

Wiki hii tunaangazia neno "Hiba" na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, katika Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, nchini Tanzania.

Bwana Sigalla anasema neno hiba lina maana mbili, moja ni kitu chochote anachopewa mtu kwa hiari au lengo la kuonyesha mapenzi, na lina maana sawa na idaya, adiya au azizi. Maana ya pili ni zawadi atoayo mtu kwa mpenzi au radhi ya mwenyezi Mungu kwetu.

Neno la wiki- Mchuuzi na Machinga

Katika neno la wiki hii leo tunaangazia maneno Mchuuzi na machinga. Mchambuzi wetu  ni Nuhu Zuberi Bakari, ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa masuala ya mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA

Bwana Zuberi anasema kwamba mchuuzi ni mtu anyeuza vitu vidogo vidogo alivyoweka sehemu iwe ni matunda, vichana au mboga alimradi anuza kwa bei ya reja reja. Machinga ni mtu yule yule anayeuza vitu vidogo vidogo lakini badala ya kuviuza katika sehemu anavibeba na kuzungusha iwe ni barabarani au kwingineko.

Neno la wiki- Mfasiri na Mkalimani

Wiki hii tunaangazia maneno Mfasiri na Mkalimani na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, katika Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, nchini Tanzania.

Bwana Sigalla anasema mfasiri ni yule anayetafsiri neno au maneno kwa maandishi na mkalimani ni mtu anayeelezea kwa mdomo maneno yanayosemwa wakati ule ule kutoka lugha moja hadi nyingine .

Neno la Wiki: Mchapalo

Wiki hii tunaangazia neno "Mchapalo" na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, katika Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, nchini Tanzania.

Bwana Sigalla anasema mchapalo ni tafrija inayofanyika ambapo wahusika wanakunywa na kula wakiwa wamesimama na kubadilishana mawazo, kwa mfano katika sentensi "Mchapalo wa uzinduzi wa vitabu ulifana sana" inamaanisha kuwa watu walikuwa wakizungumza wakibadilishana mawazo huku wakiwa wanakula na kunywa..

Neno la Wiki: SAKARANI

Wiki hii tunaangazia neno “Sakarani” na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, katika Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, nchini Tanzania.

Bwana Sigalla anasema neno Sakarani ni msamiati ya kawaida na lina maana tatu, la kwanza ni mtu asiye na akili timamu kutokana na ulevi, ya pili ni mtu ambaye amechanganyikiwa, yaani mwenye akili zisizosawa, na maana ya tatu ni mtu aliyetekwa akili zake kiasi kwamba anashindwa kuvumilia kwa sababu ya kupenda, kumaanisha mlevi wa mapenzi.