Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na wadau waomba $mil 668 kusaidia wakimbizi wa DRC

Mapigano ya kikabila huko DRC yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makwao, mathalani katika jimbo la Kalemie ambapo wakazi wake pichani wakionekana kwenye sintofahamu. (Maktaba)
UNHCR/Colin Delfosse
Mapigano ya kikabila huko DRC yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makwao, mathalani katika jimbo la Kalemie ambapo wakazi wake pichani wakionekana kwenye sintofahamu. (Maktaba)

UNHCR na wadau waomba $mil 668 kusaidia wakimbizi wa DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) kwa kushirikiana na wadau wake 105 hii leo wamezindua mpango wa kuwasaidia wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, DRC pamoja na jamii zilizowakaribisha. 

Mpango huo uliozinduliwa hii leo jijini Pretoria, Afrika Kusini utakaogharimu jumla ya dola milioni 668 kwa kipindi cha mwaka 2024-2025 unahusisha wadau kutoka nchini ambazo wakimbizi wanakimbilia kusaka hifadhi mara kwa mara kunapoibuka machafuko ambazo ni Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda, Angola, Zambia na DRC yenyewe.

Nchi hizo za jirani na DRC zinahifadhi jumla ya wakimbizi na wasaka hifadhi 950,000.

Kwa mujibu wa UNHCR nchini DRC kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 7 ambao wote wanategemea misaada ili kuendesha maisha yao wakati huu ambapo gharama za misaada ya kibinadamu zinazidi kupanda kila uchwao. 

UNHCR katika ripoti yao yameeleza kuwa fedha hizo dola milioni 668.3 zitaenda kutekeleza shughuli za kusaidia watu milioni 2 ambapo ni wakimbizi 950,000 kutoka DRC na wanajamii wanaowahifadhi wakimbizi milioni 1 katika nchi hizo saba. 

Kwa mujibu wa Muundo wa Uratibu wa Wakimbizi, serikali zinazowakaribisha wakimbizi zinasimamia utoaji wa ulinzi, usaidizi na masuluhisho ya kudumu kwa wakimbizi, wakati washirika wa RRP, wanaoratibiwa na UNHCR, wanasaidia na kukamilisha mikakati ya kitaifa na kikanda, wakifanya kazi kwa karibu na wadau wa maendeleo na sekta binafsi.

Kusoma ripoti yote kamili bofya hapa.

Hivi karibuni pia mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Bintou Keita, aliliambia Baraza la Usalama kwamba ana wasiwasi mkubwa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa unaofanywa katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23, ambapo vuguvugu hilo linalenga watendaji wa mashirika ya kiraia, hasa watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari.

Kusoma zaidi kuhusu taarifa hiyo bofya hapa.

Wakimbizi wa DRC

Mgogoro wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni mojawapo ya migogoro tata zaidi ya kibinadamu duniani. 

Miongo mitatu ya mapigano makali kati ya makundi yenye silaha, unyanyasaji ulioenea, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia (GBV), vimesababisha viwango vya juu vya mahitaji ya ulinzi na udhaifu, na kusababisha takriban watu milioni 6.2 kuyahama makazi yao ndani ya nchi na kulazimisha wengine takriban 900,000 kutafuta hifadhi kote Afrika. 

Tangu mwanzoni mwa mwaka wa 2023, hali ya ukosefu wa usalama katika mikoa ya mashariki na magharibi imeongezeka, na kusababisha ongezeko la vitendo vya uhalifu, hasa vinavyohusiana na unyanyasaji wa kijinsia, na kuzuia kwa kiasi kikubwa nafasi ya utoaji wa misaada ya kibinadamu na upatikanaji wa huduma za msingi, ambayo yote yamesababisha watu kuendelea kuhama makazi yao.

Mwezi Juni 2023, mfumo wa Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Kimataifa ulikusanyika ili kuhimiza hatua za haraka za kulinda wanawake na wasichana. 

Hali nchini humo inazidishwa na mfumuko wa bei, magonjwa ya milipuko, hatari za asili, na uhaba wa chakula.