Maisha ya maelfu ya raia wa DRC hatarini baada ya kutimuliwa Angola:UN

26 Oktoba 2018

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa serikali ya Angola kusitisha mara moja zoezi la kuwarejesha kwa nguvu maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokarasia ya Congo DRC, hadi pale itakapohakikishwa kwamba kujeresheshwa huko kunazingatia utawala wa sheria na haki za binadamu za wahamiaji.

Michelle Bachelet ametoa wito huo leo akionya kwamba kuwarejesha kwa nguvu raia hao wa DRC tayari kumeshazusha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya usalama katika pande zote mbili za mpaka na kuwaacha watu zaidi ya laki tatu waliorejeshwa katika hali mbaya.

Pia amezitaka serikali kuhakikisha kwamba vikosi vya usalama na wengine wanaohusika na ukiukwaji huo wakati wa kuwafurusha wahamiaji wanawajibishwa. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva hii leo msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani amesema

(SAUTI YA RAVINA SHAMDASAN )

“Tangu mwanzoni mwa Oktoba, watu takriban 330,000 wameripotiwa kuvuka mpaka kutoka angola na kuingia majimbo ya Kasai, Kasai Kati na  Kwango nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kufuatia amri ya serikali ya Angola ya kuwatimua wahamiaji holela.”

Familia zilizokimbia machafuko jimbo la Kasai DRC zawasili katika kituo cha hifadhi cha Lóvua, Angola. (Picha:UNHCR/Rui Padilha)
Familia zilizokimbia machafuko jimbo la Kasai DRC zawasili katika kituo cha hifadhi cha Lóvua, Angola. (Picha:UNHCR/Rui Padilha)

Ameongeza kuwa katika mahojiano na baadhi ya watu hao mpakani Kamako jimboni Kasai ofisi ya haki za binadamu imepokea tarifa zikionyeshja kwamba vikosi vya usalama nchini Angola vimekuwa vikitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wa DRC katika operesheni hiyo na kwamba

(SAUTI YA RAVINA SHAMDASAN )

“Timu imehakikishia taarifa kuhusu vifo sita, ambavyo vimeripotiwa kutokea mikononi mwa vikosi vya usalama, lakini pia imepokea madai mengine mengi ya mauaji ambayo haijaweza kuyathibitisha kikamilifu. Duru pia zinaonyesha kuwa angalau watu 100 walijeruhiwa.”

Wahamiaji kadhaa wamedai baada ya kuwasili Kamako waliporwa na kutozwa ushuru kinyume cha sheria na vikosi vya ulinzi na usalama nchini DRC. Hivi sasa Angola inahifadhi waomba hifadhi na wakimbizi 68,000.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter