Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa Ebola DRC ukitimu, mashirika ya UN yaazimia kuchukua hatua zaidi

Juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa DRC ni za pamoja. Hapa MONUSCO na UNPOL wakitoa vifaa vya kutumiwa kama vile hema, viti na vinginevyo kwa mkuu wa Polisi ya Beni kutumiwa kwa kazi hiyo.
MONUSCO / Gweny Angel Nouko
Juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa DRC ni za pamoja. Hapa MONUSCO na UNPOL wakitoa vifaa vya kutumiwa kama vile hema, viti na vinginevyo kwa mkuu wa Polisi ya Beni kutumiwa kwa kazi hiyo.

Mwaka mmoja wa Ebola DRC ukitimu, mashirika ya UN yaazimia kuchukua hatua zaidi

Afya

Kesho Agosti 1 ni mwaka mmoja tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola huko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mwaka mmoja unatimu wakati ambapo hii leo mgonjwa wa pili kuripotiwa huko Goma jimboni humo alifariki dunia, ikiwa ni wiki mbili tangu ugonjwa huo kutangazwa kuwa ni dharura ya afya ya umma inatiwa wasiwasi duniani.

Wakuu wa mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, lile la afya  ulimwenguni WHO, lile linalohusika na misaada ya dharura, OCHA na la kuhudumia watoto, UNICEF wametoa taarifa yao leo wakisema kuwa kifo cha hivi karibuni cha mgonjwa huyo ni cha pili ndani ya mwezi mmoja kwenye mji huo wa Goma wenye wakazi wapatao milioni 1.

“Kisa hiki kipya kwenye eneo hilo lenye watu wengi, kinapatia msisitizo hatari zaidi ya maambukizi ya ugonjwa huo,penginepo hata nje ya mipaka ya DRC na hivyo basi kuhitajika kwa msaada zaidi wa wahisani na kuimarisha harakati za kuudhibiti,” wamesema viongozi hao ambao ni Dkt. Tedros Ghebreyesus wa WHO, Henrietta Fore wa UNICEF na Mark Lowcock wa OCHA.

 “Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja kumekuwepo na wagonjwa 2600 waliothibitishwa kuugua Ebola wakiwemo zaidi ya 1,800 ambao wamefariki dunia kwenye jimbo la Ituri na Kivu Kaskazini. Takribani mgonjwa mmoja katika kila wagonjwa watatu ni mtoto. Kila mgonjwa ni simulizi ya machungu waliyopitia lakini zaidi ya 770 wamepona,” wamefafanua viongozi hao.

Chanjo dhidi ya Ebola  kwa wahudumu wa afya  Mashariki mwa DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
WHO-Eugene Kabambi
Chanjo dhidi ya Ebola kwa wahudumu wa afya Mashariki mwa DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Madhara ya Ebola

“Ebola huambukizwa toka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwa mume kwenda kwa mke, mgonjwa kwenda kwa mtoa huduma, kutoka mwenye maiti kwenda kwa mwili wa familia au jamaa wanaoomboleza,” imesema taarifa ya viongozi hao watatu ikiongeza kuwa, Ebola husambaratisha maisha.

Wamesema kuwa Ebola inaathiri biashara, inazuia watoto kwenda shule na kukwamisha utaratibu wa kawaida wa utoaji wa huduma za afya. “kimsingi ni janga la kafya, lakini ambalo pia linaathiri familia na jinsi watu wanahudumia familia zao, kutazama jirani zao na hata kushirikiana kwenye jamii.

Viongozi hao wamekiri kuwa changamoto za kudhibiti kusambaa zaidi kwa ugonjwa huu ni kubwa na hata hivyo hakuna changamoto yoyote inayoweza kuwa sababu ya kuzuia kazi hiyo.

Watoto wa shule sehemu za Beni -DRC wajifunza kuwa kuosha mikono ndiyo njia bora ya kujilinda dhidi ya Ebola
UNICEF/Thomas Nybo
Watoto wa shule sehemu za Beni -DRC wajifunza kuwa kuosha mikono ndiyo njia bora ya kujilinda dhidi ya Ebola

Harakati za kudhibiti Ebola

Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaendelea kuimarisha juhudi za kusaidia serikali ya DRC na inaweka mazingira bora ili operesheni za kiafya ziweze kuendelea ikiwemo hatua sahihi za kiulinzi, na ushiriki wa jamii na viongozi katika ngazi mbalimbali.

“Tunapongeza pia juhudi za kishujaa za wahudumu wa afya wa DRC walio mstari wa mbele kukabilia na ugonjwa huu. Hata hivyo licha ya juhudi zao bado ugonjwa unaendelea kusambaa. Mlipuko huu upo kwenye eneo lenye mapigano na hivyo kukwamisha juhudi zetu za kukabili Ebola,” wamesema viongozi hao wa OCHA, UNICEF na WHO.

 Kwa mantiki hiyo basi, “tunatoa wito kwa pande husika kwenye mzozo kuhakikisha kuwa watoa huduma za afya wanaweza kufanya kazi yao kwa usalama na wale wanaosaka huduma waweze kuipata bila uoga wala kushambuliwa,” wamesema.

 

KILICHOFANYIKA HADI SASA

  • Zaidi ya watu 170,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola
  • Watu 1,300 walipatiwa matibabu kwenye vituo 14 kwa kutumia dawa za majaribio dhidi ya Ebola
  • Wasafiri milioni 77 million wa kitaifa na kimataifa walichunguzwa dhidi ya Ebola
  • Watu 20,000 walitembelewa kila siku kuchunguzwa baada ya kuwa na makaribiano na wagonjwa wa Ebola ili kuhakikisha kuwa hawaugui ugonjwa huo
  • Sampuli 3,000 za zilichunguzwa kila siku  katika maabara 8
  • Kulikuwepo na zaidi ya maeneo 10,000 ya kunawa mikono hasa kwenye maeneo yaliyokuwa na hatari zaidi
  • Zaidi ya wafanyakazi 2,000 wa kijamii walifanya kazi kwenye maeneo yaliyoathirika ili kusikiliza hofu za wanajamii, kujenga imani na kuhamasisha ushiriki kwenye kampeni dhidi ya Ebola
  • Kila siku wanafunzi 25,000 walio kwenye maeneo hatarishi na Ebola walipatiwa mlo kila siku