Guterres akielekea DRC, kisa kipya cha Ebola chabainika Uganda

30 Agosti 2019

Wakati idadi ya wagonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imevuka 2000, mgonjwa wa Ebola amebainika kwenye nchi jirani ya Uganda, limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO hii leo. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Taarifa hizi zimekuja wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akielekea DRC kuonyesha mshikamano na manusura, waathirika na watoa huduma dhidi ya Ebola.

Msemaji wa WHO huko Geneva, Uswisi, Fadela Chaib amesema mgonjwa huyo ni mtoto ambaye alikuwa amesimamishwa kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida mpakani huko Mpondwe magharibi ya Uganda. “Mtoto huyo wa kike ana umri wa miaka 9, ni raia wa DRC alibainika na Ebola Uganda kwa hiyo alikwenda DRC kusaka matibabu ya Ebola akiwa kwenye bodaboda. Hatufahamu kama bado ni mzima au la. Sina taarifa za matibabu, ninachofahamu ni kwamba alifika mpakani akiwa na dalili zote za Ebola, alikuwa anatoka damu mdomoni, alikuwa na vipele na homa.”

 Tayari mamlaka Uganda zimechukua hatua wakati huu ambapo huko DRC watoto wanazidi kuathirika zaidi na Ebola.

Shirika la Umoja wa Mataifa  la kuhudumia watoto, UNICEF limesema takribani watoto 600 wamefariki dunia kutokana na Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC tangu ugonjwa huo ulipuke kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri mwezi Agosti mwaka jana.

Huyu ni Stephanie, mtoto yatima, mama yake alifariki kwa Ebola  huko Mangina jimboni Kivu Kaskazini.

©UNICEF/Thomas Nybo
Kampeni dhidi ya Ebola ambako wahamasishaji wanajibu maswali ya wanajamii huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC. (Agosti 2019)

UNICEF inasema Stephanie na watoto wengine wengi wamesalia yatima wakati huu ambapo idadi ya vifo vya Ebola ikivuka 2000, kati ya visa 3000 vilivyoripotiwa.

Watoto 850 ndio waliambukizwa na 600 wamefariki dunia.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC Edouard Beigbeder, amesema mwelekeo wa maambukizi ya Ebola pamoja na vifo ni ishara ya kuchukua hatua zaidi ili kutokomeza ugonjwa huo akisisitiza kuwa hatua zozote za kinga lazima zizingatie mahitaji pekee ya watoto.

Hivyo amesema “kadri idadi inavyoongezeka ni lazima tukumbuke kuwa wagonjwa hao ni mtoto, mama, baba, binti, kaka au dada wa mt una kila kifo kinaacha familia na huzuni lakini pia hofu ya kwamba nao pia wameambukizwa ugonjwa.”

Kazi ya kinga na tiba ikiendelea, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP nalo linaendelea kusambaza vifaa vya misaada.

Msemaji wa WFP Herve Verhoosel amesema wanatoa misaada ya usafiri, bohari za kuhifadhi vifaa na miundombinu mingine na kwama wamejenga kambi tatu kwa ajili ya watoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud