Mgonjwa wa pili wa Ebola Goma, akifariki dunia, WHO yaimarisha hatua kudhibiti ugonjwa huo

31 Julai 2019

Mgonjwa wa pili wa Ebola aliyebainika na kuthibitishwa jana huko Goma jimboni Kivu, Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amefariki dunia.

Hii ni kwa muijbu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na mratibu wa hatua za dharura dhidi ya Ebola nchini humo, David Gressly, na Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa shirika la afya duniani WHO kuhusu hatua za dharura Dkt. Ibrahima Socé Fall.

Hata hivyo taarifa yao imesema kuwa wanafanya kila liwezekanalo kuchukua hatua zote za tahadhari ili kuzuia kusambaa zaidi kwa Ebola mjini Goma wakati huu ambapo kesho Agosti Mosi ni mwaka mmoja tangu kuanza kwa mlipuko wa 10 wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.  

Wameongeza kuwa hadi sasa hakuna ushahidi kwamba mgonjwa huyo alikuwa na uhusiano wowote na mgonjwa wa awali ambaye alikuwa mchungaji wa kanisa aliyesafiri kwenda Goma akitokea Butembo.

Kwa mujibu wa taarifa yao mgonjwa huyu wa pili ambaye ameshafariki dunia ni mchimba madini aliyekuwa anafanya kazi kwenye mgodi mmoja huo jimboni Ituri na alisafiri kurejea nyumbani Goma Julai 13.

Uchunguzi katika kila kona ya mpaka na sehemu watu wanakoingilia umeimarishwa na jamii ikishirikishwa katika kampeni hiyo lakini pia matangazo ya hatari ya kusambaa kwa mlipuko huko na tahadhari yza kuchukua yakisambazwa kila kona.

Hata hivyo WHO inasema kisa hiki kipya Goma ni uthibitisho kwamba ingawa kumekuwa na hatua kubwa katika kupambana na kusambaa kwa Ebola juhudi zaidi zinahitajika na kusistiza kwamba juhudi za kukomesha mlipuko wa Ebola ni lazima ziendelee hadi pale watakapohakikisha hakuna kisa kingine tena.

Maafisa hao wamesema pia ni lazima kuhakikisha kuna mifumo ya afya ambayo ni imara na yenye mnepo inayoweza kusaidia kuepuka kuzuka upya kwa mlipuko wa Ebola DRC.

Wameipongeza serikali ya DRC kwa hatua inazochukua ili kusaidia juhudi za WHO za kutaka kukomesha mlipuko wa sasa wa Ebola nchini humo.

Bwana Gressly na Dkt. Fall pia wamewasifu wahudumu wa afya ambao wanahatarisha maisha yao wakiwa msitari wa mbele kuhakikisha kila juhudi inafanyika kumaliza mlipuko wa Ebola DRC.

Wametoa wito kwa wadau wa kimataifa na wahisani kuendelea kutoa msaada na kushiriki kikamilifu katika juhudi zinazoendelea ili kumaliza mlupuko huu wa Ebola katika taifa ambalo tayari limelemewa na changamoto kubwa ya vita.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter