Muhula mpya wa shule waanza DRC, UNICEF yachukua hatua kulinda watoto

3 Septemba 2019

Mhula mpya wa shule ukianza huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake wamekuwa wakitathmini mahitaji ya kiafya na huduma za kujisafi ili kuepusha kuenea kwa Ebola. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, Dakar Senegal na Kinshasa, DRC inasema kuwa takribani watoto milioni 2 wanaoishi kwenya meneo yaliyoathirika kwa Ebola huko mashariki mwa DRC wanarejea shuleni.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC Edouard Beigbeder amesema kuwa ugonjwa huo umekuwa na madhara makubwa kwa watoto na familia zao pamoja na jamii kwa hiyo usaidizi ni muhimu ili waweze kurejea kwenye mazingira salama shuleni na waweze kuendelea kusoma.

Kuna jumla ya shule za msingi na sekondari kwenye majimbo ya Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini ambayo yamekumbwa ambapo kati ya shule hio, 3800 ziko kwenye maeneo yaliyo hatarini zaidi kutokana na mlipuko wa Ebola kuwa ni mkubwa.

Kwa mantiki hiyo UNICEF inachofanya sasa ni kubaini ni shule zipi ambazo zinahitaji vifaa vya kujisafi na usafi pamoja na huduma za afya huku ikiimarisha vikasha vya taarifa na miongozo ya kupambamba na Ebola kwa kuzingatia taarifa wanazopokea kutoka kwa walimu.

Vifaa vinavyohusika ni vipimajoto, maeneo ya kunawa mikono na vikasha vya kuelimisha kuhusu dalili za Ebola na jinsi ugonjwa huo unavyoenezwa.

Bwana Beigbeder pamoja na vifaa walimu nao wamepatiwa mafunzo ya kusaidia watoto kisaikolojia kwa kutambua kuwa baadhi ya watoto wanaorejea shuleni wameathirika kwa Ebola, iwe kwa kupoteza wazazi,jamaa au wao wenyewe kuwa ni manusura wa Ebola.

Amesema watoto wanakabiliwa na ubaguzi au unyanyapaa.

Hata hivyo yaelezwa kuwa hali ya mwaka huu ni nafuu zaidi kuliko mwaka jana ambapo Fati Bagna wa kitengo cha elimu UNICEF anasema wazazi mwaka jana waliogopa kupeleka watoto wao shuleni kwa hofu ya kuambukizwa.

Hata hivyo elimu iliyotolewa na UNICEF na wadau imepunguza hofu na wazazi wanapeleka watoto wao shuleni.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter