Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya vifo vya Ebola ikiongezeka DRC, Guterres apaza sauti

Katika kliniki moja  ya kutibu wagonjwa wa Ebola huko Mbandaka jimbo la Kivu Kaskazini, mhudumu akiwa amevalia mavazi rasmi ili kuepusha maambukizi.
Shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu na hilal nyekundu
Katika kliniki moja ya kutibu wagonjwa wa Ebola huko Mbandaka jimbo la Kivu Kaskazini, mhudumu akiwa amevalia mavazi rasmi ili kuepusha maambukizi.

Idadi ya vifo vya Ebola ikiongezeka DRC, Guterres apaza sauti

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya idadi mpya ya wagonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York, Marekani hii leo, Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea na jitihada zake za kudhibiti Ebola huko Kivu Kaskazini nchini DRC.

Ripoti zinasema kuwa mwezi 10 sasa tangu mlipuko wa ugonjwa huo zaidi ya watu 1000 wamefariki duniani ambapo Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa.

Hata hivyo Bwana Guterres amepongeza serikali ya DRC, taasisi zake na wananchi kwa hatua za kudhibiti ugonjwa huo ambao ulikumba pia jimbo la Ituri.

Taswira kutoka angani ya eneo la Butembo jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  DRC ambako tarehe 19 mwezi Aprili 2019, watu wenye silaha walishambulia kliniki ya Ebola na kumuua Dkt. Richard Mouzoko.
WHO/Junior Kannah
Taswira kutoka angani ya eneo la Butembo jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako tarehe 19 mwezi Aprili 2019, watu wenye silaha walishambulia kliniki ya Ebola na kumuua Dkt. Richard Mouzoko.

Amewapongeza pia wafanyakazi wa usalama, afya na watoa huduma za kibinadamu akisema, “wameweka rehani maisha  yao katika mazingira magumu ili kuokoa maisha ya wengi.”

Bwana Guterres amesema eneo husika lina changamoto za usalama ikiwemo mashambulizi kwenye vituo vya kutibu Ebola na vituo vya huduma za afya.

“Hadi sasa kupitia zao, zaidi ya watu 100,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola na hivyo kuokoa maisha ya mamia ya watu ambao vinginevyo wangaliambukizwa Ebola,” amesema Katibu Mkuu.

Rasilimali zaidi zahitajika kudhibiti Ebola

Wakati huu ambapo kuna mabadiliko ya mwelekeo wa kutibu Ebola huko DRC, Katibu Mkuu amesisitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa kuwa na mwelekeo mmoja wa utekelezaji, kuanzia Kinshasa ambako UN inaongozwa na mwakilishi wake maalum na katika maeneo yenye mlipuko ambako hatua za utekelezaji zinaongozwa na shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Hata hivyo amesema ushiriki wa jamii mashinani katika vita dhidi  ya Ebola unasalia muhimu sana kwenye harakati za kudhibiti mlipuko huo ambao ni wa pili kwa ukubwa katika historia ya DRC.

Katibu Mkuu amesihi viongozi wote nchini DRC washirikiane bila kujali vyama vyao vya siasa au jamii zao ili kutokomeza Ebola.

Amekumbusha pia katika hali ya sasa rasilimali zaidi zahitajika hivyo amesihi nchi wanachama na jamii ya kimataifa na wadau wasaidie kupatikana kwa rasilimali zinazohitajika.