Tuongezeeni nguvu ili tukabiliane vyema na Ebola DRC- WFP

24 Aprili 2019

Wakati Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC ikipambana na mlipuko wa Ebola ambao ni wa pili kwa ukubwa katika historia ya nchi hiyo, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limetahadharisha hii leo mjini Goma kuwa rasilimali zinazohitajika kusaidia shughuli zake, haziendani na kasi ya ongezeko la hivi karibuni la maambukizi na uwepo wa hatari ya kusambaa kwa virusi hivyo ndani ya DRC na katika nchi za jirani.

Operesheni za WFP ni pamoja na kusaidia kudhibiti Ebola kwa kutoa chakula kwa watu ambao wanasadikika kuwa na virusi vya Ebola na pia kutoa huduma nyingine muhimu zikiwemo usafiri wa anga ambao unawawezesha maafisa wa kuudhiti ugonjwa huo kuweza kufika kwa haraka katika maeneo mapya au yale yasiyofikika kwa urahisi.

Hata hivyo Kamati ya dharura iliyoitishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani WHO ilieleza wasiwasi kuhusu ongezeko la maambukizi katika maeneo mahususi na uwezekano wa kusambaa katika nchi za jirani.

Pia katika wiki chache zilizopita kumeshuhudiwa kudorora kwa usalama katika maeneo yenye Ebola hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa na wahudumu wao. Juma lililopita mtaalamu mmoja wa afya Dkt Richard Valery Mouzoko Kiboung wa WHO aliuawa katika shambulizi lililofanyika katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Butembo, wengine wawili walijeruhiwa katika shambulio hilo.

Mkurugenzi wa WFP nchini DRC Claude Jibidar anasema, “mlipuko wa Ebola ni janga ambalo linatokea katika mgogoro mwingine mkubwa wa kibinadamu nchini DRC ambako WFP inatoa msaada wa kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni 5. Ili kumudu operesheni hizi mbili kwa pamoja tunahitaji haraka nyongeza ya rasilimali.”

Pia Jibidar anaeleza namna msaada wa chakula unavyosaidia kufanikisha kudhibiti Ebola, “Vifurushi vya chakula ambavyo vinatolewa na WFP na wadau wake, vinamaanisha kuwa wale ambao wana virusi vya Ebola hawahitaji kutoka katika nyumba zao kwenda kununua chakula. Watu wanaopokea chakula wanajitolea kujiandikisha, kuchanjwa na kupatiwa matibabu.” Anasema Jibidar.

Kwa ajili ya operesheni za WFP nchini DRC, shirika hilo linahitaji dola milioni 20.5 kwa miezi mitatu ijayo na hadi kufikia sasa wamepokea dola milioni 6 pekee.

Wakati sasa msisitizo ni kuzuia Ebola kutoingia katika maeneo mengine ya DRC, WFP pia inazisaidia nchi za jirani kama Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi na Tanzania ili kujiandaa ikiwa ugonjwa huo utasambaa.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter