Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwitikio wa wananchi kwenye harakati dhidi ya Ebola huko Katwa na Butembo watia moyo- WHO

Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.

Mwitikio wa wananchi kwenye harakati dhidi ya Ebola huko Katwa na Butembo watia moyo- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema linatiwa matumaini makubwa na harakati za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola huko jimboni Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Taarifa ya WHO kutoka Geneva, Uswisi inasema shirika hilo linatiwa moyo zaidi kutokana na kuongezeka kwa mwitikio wa jamii katika kushiriki kwenye kampeni hizo licha ya changamoto zinazoendelea za ukosefu wa usalama kutoka vikundi vilivyojihami.

Mathalani imesema katika siku 21 zilizopita, huko Katwa na Butembo, asilimia 88  ya familia 256 ambazo zilikuwa na mgonjwa aliyefariki dunia na kushukiwa kuwa na Ebola, zilikubali msaada kutoka wahudumu wa afya wanaoendesha operesheni dhidi ya Ebola, msaada ambao ni kuzika kwa heshima na utu wagonjwa waliofariki dunia.

Halikadhalika, chanjo ya mzunguko dhidi ya Ebola imefanyika kwenye eneo hilo kwa asilimia 74 ambapo zaidi ya asilimia 90 ya watu waliokuwa wanapaswa kupatiwa chanjo hiyo walikubali na zaidi ya asilimia 90 walishiriki katika hatua ya marejeo kutoka kwa watoa huduma ya afya.

WHO inasema maabara saba zilizoko mashinani huko Butembo na Katwa zinaendelea kufanya kazi na wahusika wanaendelea kuchukua sampuli ili kubaini kama kuna virusi au la.

“Katika wiki iliyopita, sampuli 1213 kutoka kwa wagonjwa shukiwa wapya zilichukuliwa na wahudumu wetu wa kujitolea wamefikia kaya 6000,” imesema taarifa ya WHO.

Awali pamoja na changamoto ya ukosefu wa usalama, jamii nayo ilikuwa haina imani na watoa huduma.

Mlipuko huu wa sasa wa Ebola ulioanza mwaka jana kwenye jimbo la Ituri na kisha Kivu Kaskazini umetajwa kuwa ni mlipuko wa pili kwa ukubwa katika historia ya milipuko ya Ebola nchini DRC.