Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya wanawake ni kizingiti cha haki za binadamu:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. Picha: UM

Ukatili dhidi ya wanawake ni kizingiti cha haki za binadamu:Guterres

Kila mwanamke na msichana ana haki ya kuishi maisha huru bila ukatili , lakini bado ukiukwaji wa haki za binadamu unatokea katika njia mbalimbali kwenye jamii na kuathiri hususani makundi ya wasiojiweza na waliotengwa ukiwemo ukatili dhidi ya wanawake. John Kibego na taarifa kamili.

(TAARIFA YA KIBEGO)

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani wakati wa tukio la kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

Amesema duniani kote zaidi ya mwanamke 1 kati ya 3 anakabiliwa na ukatili katika maisha yake yote, ambapo wanawake milioni 750 wakiolewa chini ya umri wa miaka 18, wengine zaidi ya milioni 250 wamepitia visu vya ngariba katika ukeketaji, huku wanawake wanaharakati wa haki za binadamu wakishambuliwa kwa kiwango cha juu na kuongeza kuwa

(GUTERRES CUT 1)

“Ukatili huu ni ishara ya wazi ya mfumo dume unaoenea na kuathiri moja kwa moja wanawake afya ya kimwili na kisaikolojia. Pia huathiri familia, jumuiya na jamii, na ukiendelea hatutoweza kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.”

image
Walinda amani wanawake wakizunugmza na wanawake wanajamii eneo la Ntoto Kivu Kaskazini.(Picha:MONUSCO)
Hivyo amesisitiza

(GUTERRES CUT 2)

“Ni wakati wa kuongeza hatua yetu ya pamoja ili kutokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Hii inahitaji sisi sote kufanya kazi pamoja katika nchi zetu wenyewe, kanda zetu  na jamii, na wakati huo huo, kuelekea lengo moja.”

Amesema haki za binadamu haziwezi kutimilika endapo ukatili dhidi ya wanawake katika kila nyanja ukiwa bado unaendelea. Siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake huadhimisha kila mwaka Novemba 25.