Haki ya tiba yaongeza wanaopata dawa kupunguza makali ya VVU-Ripoti

20 Novemba 2017

Kuelekea siku ya Ukimwi duniani tarehe mosi mwezi ujao, imeelezwa kuwa takribani watu milioni 21 hivi sasa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU wanapatiwa matibabu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya Ukimwi, UNAIDS limesema hay oleo katika ripoti yake mpya ikisema idadi hiyo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na watu 685,000 mwaka 2000.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé, amesema siri ya mafanikio ni ujasiri wa watu wanaoishi na VVU kudai haki yao ya msingi ya matibabu, sambamba na uongozi thatbiti na ufadhili wa kifedha.

Ametolea mfano Afrika Kusini akisema ina mpango madhubuti wa kuokoa maisha ya watu wenye VVU ambapo watu milioni 4 wanapata dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.

Bwana Sidibé amesema kasi ya matumizi ya dawa hizo inaonyesha pia wale wanaozitumia wanaweza kwa asilimia 97 kuzuia mambukizi mapya.

Hata hivyo amesema changamoto sasa ni kuhakikisha watu milioni 17 wenye VVU wanapatiwa dawa ikiwemo watoto 919 000.