Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usaidizi waendelea kwa manusura wa tetekemo la ardhi Iran na Iraq

Eneo lililotokea tetemeko la ardhi mpakani mwa Iraq na Iran. Picha: OCHA

Usaidizi waendelea kwa manusura wa tetekemo la ardhi Iran na Iraq

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limeendelea kupeleka vifaa vya matibabu kwa manusura wa tetemeko la ardhi mpakani mwa Iran na Iraq.

Vifaa vya hivi karibuni zaidi ni vile vya kusaidia matibabu ya maelfu ya watu waliojeruhiwa na kukumbwa na kiwewe baada ya mkasa huo wa jumapili jioni.

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na masuala ya dharura kwenye ukanda huo Dkt. Michel Thieren amesema vifaa hivyo vitatosheleza matibabu kwa watu 4,000 na misaada zaidi inasafirishwa kutoka bohari ya shirika hilo huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Amesema ingawa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya tetemeko la ardhi na mlipuko wa magonjwa, bado WHO inafuatilia kwa karibu uwezekano wa uwepo wa visa vya magonjwa ya maambukizi hasa yale yanayoambukizwa kwa njia ya matumizi ya maji machafu.

Takribani watu 9400 nchini Iran walijeruhiwa kutokana na tetemeko hilo la ardhi ilhali kwa upande wa Iraq madhara yalikuwa makubwa zaidi ambapo watu 8 walifariki dunia na wengine 525 walijeruhiwa.