Mamlaka ya uhamiaji Libya msikiuke haki za binadamu: Zeid
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein leo ameonyesha wasiwasi wake kutokana na ongezeko kubwa la wahamiaji walio vifungoni katika vituo mbalimbali nchini Libya, akisema sera ya Umoja wa Ulaya ya kusaidia ulinzi wa pwani ya Libya ili kuzuia wahamiaji kuingia barani humo inakiuka haki za binadamu.
Bwana Zeid amesema mateso ya wahamiaji waliofungwa Libya ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu na kinyume cha ustaarabu kwa mtu yeyote, huku akiongeza kuwa njia mbadala za kuwekwa kizuizini zinaweza kuokoa maisha ya wahamiaji na usalama wao kimwili, pia kuwalinda kutokana na mateka toka kwa wanamgambo.
Aidha Bwana Zeid amesema kuwa jumuiya ya kimataifa haitaendelea kufumbia macho hali ya wahamiaji huko Libya, huku akitaka kuundwa kwa hatua za kisheria ili kuboresha sera za uhamiaji ili kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu unatekelezwa Libya.
Kulingana na takwimu ya idara ya kupambana na uhamiaji haramu Libya (DCIM) watu 19,900 wako chini ya udhibiti wa idara hiyo tangu mapema mwezi huu ikiwa ni idadi kubwa ikilingannishwa na watu 7,000 Septemba wakati wa migogoro ya huko Sabratha.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa inashauri mamlaka ya Libya kuchukua hatua thabiti ili kuondokana na ukiukwaji wa haki za binadamu katika vituo vya uthibiti wa wahamiaji nchini humo.