Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL ni lazima ikabiliwe na makosa ya uhalifu wa kimataifa: UM

ISIL ni lazima ikabiliwe na makosa ya uhalifu wa kimataifa: UM

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kufuatia ukombozi wa mji wa Mosul nchini Iraq inasema kundi la kigaidi la ISIl au Daesh lilitekeleza vitendo vya ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu ambavyo ni uhalifu wa kimataifa katika kipindi cha miezi tisa ya kampeni ya kijeshi ya ukombozi wa mji huo.

Ripoti hiyo iliyochapishwa leo na mpango wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Iraq UNAMI na ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imetokana na maelezo ya mashahidi na nyaraka zinazoelezea utekwaji wa kundi kubwa la raia, matumizi ya maelfu ya watu kama ngao, urushaji wa makusudi wa makombora kwenye makazi ya raia  na mashambulizi ya kupangwa dhidi ya raia waliokuwa wakijaribu kukimbia Mosul.

Mwezi Julai mwaka huu vikosi vya serikali ya Iraq ISF na makundi yenye silaha yanayowaunga mkono walifanikiwa kuukomboa mji wa Mosul uliokuwa ukidhibitiwa na kundi la ISIl tangu  Juni mwaka 2014.

Kwa mujibu wa Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein, wakati wa operesheni ya ukombozi wa Mosul maelfu ya raia walikabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa katika mikono ya ISIL akisisitiza kuwa watekelezaji wa ukiukwaji huo ni lazima wawajibishe.