Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chile yaingia katika orodha ya kuhifadhi wakimbizi wa Syria:UNHCR

Chile yaingia katika orodha ya kuhifadhi wakimbizi wa Syria:UNHCR

Chile imekuwa taifa la karibuni kuwapa makazi wakimbizi wa Syria. Jumla ya wakimbizi 66 wakiwemo watoto 32, wanawake 16 na wanaume 18 waliwasili jana nchini humo kutokea Lebanon kama sehemu ya mpango wa kuwapa wakimbizi makazi unaongozwa na serikali ya Chile kwa msaada wa shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Mjini Santiago wakimbizi hao walilakiwa na rais Michelle Bachelet , mwakilishi wa kikanda wa UNHCR Michele Manca di Nissa na watu wengine. Wakimbizi hao watahifadhiwa katika jamii mbili tofauti kwenye eneo la Villa Alemana, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo na eneo la Macul katikati Mashariki mwa mji wa Santiago.

Mwakilishi wa UNHCR Bi Manca di Nissa ameipongeza serikali ya Chile na jamii nzima kwa ukarimu wao, kwa kuitikia wito wa jumuiya ya kimataifa  na kushikamana na wakimbizi hao wanaohitaji msaada kutokana na janga kubwa la kibinadamu tangu vita ya pili ya dunia.