Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tabianchi isipodhibitiwa ajenda 2030 itakuwa ni ndoto- Guterres

Tabianchi isipodhibitiwa ajenda 2030 itakuwa ni ndoto- Guterres

Ajenda ya maendeleo endelevu, SDGs itasalia ndoto kwa nchi ambazo kila wakati zinakabiliwa na mafuriko na ujenzi wa miundombinu iliyosambaratishwa na majanga hayo ya asili.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwenye kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika makao makuu ya Umoja huo jijini NewYork, Marekani kikiangazi dhoruba Irma iliyoleta maafa kwenye ukanda wa Karibea.

Bwana Guterres amesema dhoruba hiyo pamoja na kusababisha vifo, imeacha mamilioni ya watu katika sintofahamu akisema muarobaini ni kuchukua hatua kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hali za tabianchi zisizo na vipimo zinahusishwa na dhoruba kali Karibea, mafuriko Asia na ukame na njaa Afrika akisema madhara yake yanakwamisha harakati za nchi kutekeleza SDGs au ajenda 2030.

Kwa mantiki hiyo amesema..

“Iwapo hatutajiandaa vema kukabili dhoruba, kupunguza athari zake na kujenga uwezo wa kukwamuka, dhoruba hizo zitaendelea kuleta machungu kwa jamii, visiwa n ahata nchi nzima, na kutwamisha maendeleo ya kilimo na kiuchumi ambayo yameshapatikana.”

Katibu Mkuu amesema taasisi za fedha zina dhima muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo akipongeza Benki ya Dunia kwa ushiriki wake katika mkutano wa leo.