Watoto wawataka viongozi wa kisiasa kumaliza vita yei:UNMISS

17 Julai 2017

Watoto wanaokabiliwa na madhila makubwa kutokana na vita vinavyoendelea Sudan Kusini na umasikini wamewataka viongozi wa kisiasa kurejesha amani kwenye mji wa Yei nchini humo.

Kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS, hali ni mbaya jimboni Yei, asilimia 70 ya watu walikimbia mwaka jana baada ya machafuko kuzuka baina ya serikali na majeshi ya upinzani na kuuacha mji huo kuwa mahame.

Hivi sasa kuna dhiki ya chakula na wakulima hawawezi kufuatilia mazao yao kutokana na kutukuwepo usalama unaojumuisha mauaji, utekaji, ubakaji na uporaji.

Hata hivyo baadhi ya watoto bado wamesalia kwenye jimbo hilo wakiwemo watoto yatima wanaohifadhiwa katika shule ya msingi ya Katoliki ya Christ the King.

Mmoja wa watoto hao ni Ester Quintin ambaye amesema “wazazi wangu wote wamekufa, marafiki zangu wote wamekufa, sina mtu yoyote wa kunisaidia katika elimu yangu , sina chochote cha kula au fedha za kusaidia elimu yangu”.

Na hii ni hadithi ya watoto wengi katika eneo hilo ambao sasa wanasema wamechoshwa na vita na wanachohitaji ni amani na viongozi wa kisiasa washike usukani katika hilo.

Mkuu wa UNMISS David Shearer, hivi karibuni amekutana na viongozi wa kisiasa, wa kidini na kijamii kujadili hali ya usalama katika eneo hilo.