Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna matumaini Cyprus licha ya ugumu uliopo- Guterres

Kuna matumaini Cyprus licha ya ugumu uliopo- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameshiriki mkutano wa kimataifa kuhusu Cyprus na kuonyesha kuwepo na matumaini kwa nchi hiyo kurejea tena katika taifa moja.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Crans-Montana nchini Uswisi baada ya kuongoza mkutano huo, Bwana Guterres amenukuu washiriki wa mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana wakieleza kuwa wote wana nia ya kupata suluhu ya kudumu.

Amesema ni dhahiri shairi kuwa kuna masuala nyeti ya kuafikiana kama vile usalama baina ya jamii mbili ambazon ni raia wa Cyprus wenye asili ya Uturuki na wale wenye asili ya Ugiriki, hivyo amesema..

“Hakuna shaka kuwa baadhi ya mambo nyeti na magumu bado hayajapatiwa suluhu. Suala la usalama na ibara inayohusu hakikisho ni muhimu ili kufikia suluhu ya kudumu. Majadiliano ya siku chache zilizopita yameonyesha tena kuna azma ya kusaka suluhu zinazokubalika pande zote kuhusu usalama na suala la hakikisho kwa jamii zote mbili. Lakini ni dhahiri kuwa usalama wa jamii moja hauwezi kukamilika kwa kuweka jamii nyingine hatarini.”

Bwana Guterres amewashukuru viongozi wa pande mbili hizo ambao ni kiongozi wa Cyprus ya Ugiriki Nicos Anastasiades na yule wa Cyprus ya Uturuki Mustafa Akinci pamoja na wadhamini wao watatu, Ugiriki, Uturuki na Uingereza huku Muungano wa Ulaya ukiwa ni mtazamaji.

Kisiwa cha Cyprus kilicho kwenye bahari ya Mediteranea kiligawanyika mapande tangu mwaka 1974.