Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza kwa watoto masikini kuna thamani kubwa: UNICEF

Kuwekeza kwa watoto masikini kuna thamani kubwa: UNICEF

Kuwekeza katika afya kwa watoto masikini na jamii zao kuna thamani kubwa, na kunaokoa maisha karibu mara mbili kwa kila dola milioni moja zinazotumika kama uwekezaji mbadala kwa makundi yasiyojiweza. Hii ni kwa mujibu wa uchambuzi mpya wa utafiti uliotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF hii leo.

Utafiti huo unaonyesha kwamba uboreshaji wa huduma za afya kwa makundi yasiyojiweza kunasaidia kupunguza haraka vifo vya watoto mara tatu zaidi ukilinganisha na makundi mengine. Pia unasema bila kupiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto basi ifikapo mwaka 2030 karibu watoto milioni 70 watafariki dunia kabila ya kufikisha miaka mitano ya kuzaliwa.

Miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano ni Afghanistan, Bangladesh na Malawi ambako kuwekeza kwa watoto masikini kumeleta tofauti kubwa. Joster Banda ni mratibu wa masuala ya afya wilaya ya Kassungu nchini Malawi

(JOSTER BANDA CUT)

"Kwa sababu ya usimamizi jumuishi wa visa vya afya katika jamii (ICCM) unaotolewa na wasaidizi wa ufuatiliaji wa afya katika wilaya ya Kasungu, tumeweza kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka 5 kwa nusu, kutoka 133 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa mwaka 2010 hadi 60 kwa kila 1000 mwaka 2015, Hivyo nadhani ICCM imechangia sana katika wilaya yetu"

Utafiti huo umependekeza masuala sita ya kuzingatia ambayo ni kutumia vyandarua vya mbu vilivyowekwa dawa, kunyonyesha watoto miezi ya mwanzo, kupewa chanjo, kupatiwa huduma na wataalamu wakati wa kujifungu, na kutibu ipasavyo maradhi kama kuhara, homa na kichomi kwa watoto