Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 130 wahofiwa kufariki dunia baharini Mediteranea

Watu 130 wahofiwa kufariki dunia baharini Mediteranea

Watu wapatao 130 wanahofiwa kufa maji katika bahari ya Mediteranea baada ya boti tatu kuripotiwa kuharibika majini na kuzama usiku wa Jumatatu.

Shirika la wakimbizi duniani, UNHCR limesema tukio la kwanza linahusisha boti iliyoondoka Libya tarehe 15 mwezi huu ambapo manusura wamesema ilikuwa na watu 133 na hadi sasa 129 hawajulikani walipo.

Tukio la pili ni boti iliyokuwa na watu 85 ambayo ilipasuka na kuzama jana ikiripotiwa kuwa na idadi kubwa ya watoto.

UNHCR imesema tukio la tatu boti imepotea na watu saba hawajulikani waliko au wamefariki dunai.

Cecily Pouilly ni msemaji wa UNHCR Geneva.

(Sauti ya Cecile)

“ Matukio haya yanatukumbusha kuwa hatari ambazo watu wanakumbana nazo wanapolazimika kukimbia makwao kwa sababu ya vita, mateso.”