Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu pekee ya vita Afghanistan ni amani-Guterres

Suluhu pekee ya vita Afghanistan ni amani-Guterres

[caption id="attachment_320711" align="aligncenter" width="615"]03hapanapaleguteres

Vita nchini Afghanistan suluhu yake sio mtutu wa bunduki, amesema Jumatano Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipotoa wito kwa pande kinzani nchini humo kusaka kwa pamoja suluhu ya kiasa ya vita vinavyoendelea.

António Guterres amefanya ziara ya kwanza nchini humo kama Katibu Mkuu ambako amekutana na maafisa wa serikali na watu waliotawanywa na machafuko hivi karibuni. Vifo vya raia nchini Afghanistan mwaka jana vilifurutu ada kuanzia vitokanavyo na mashambulizi ya kujitoa muhanga, na mengine yanayoendeshwa na wapiganaji wa itikadi kali wa Taliban, imesema ripoti ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA).

Guterres amewasili Afghanistan Jumatano ili kuonyesha mshikamano na watu wa taifa hilo katika wakati huu ambao wameghubikwa na vita na madhila mengi.

Pia ametangaza kwamba anafunga katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kwa kuheshimu utamaduni na dini kwa watu wa Afghnaistan na jamii ya Kiislam kote duniani. Ziara ya Guterres imeanza kwa kukutana na watu waliotawanywa na machafuko nje kidogo ya mji mkuu Kabul.

(SAUTI YA GUTERRES)

"Ni dhahiri kwamba amani ndio suluhu ya matatizo yao, na jumuiya ya kimataifa , nchi jirani, na wote ambao wanaohusiana na mzozo wa Afghanistan wanahitaji kuelewa kwamba , hivi ni vita suluhu yake sio ya kijeshi, na kwamba tunahitaji kuwa na suluhu ya kisiasa.”

Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kibinadamu kwa watu wa Afghanistan na kuweka mazingira ya watu hao kuishi kwa utu.