Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen si makazi salama kwa mtoto- UNICEF

Yemen si makazi salama kwa mtoto- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema Yemen hivi sasa si pahala salama kwa makuzi ya mtoto kwa kuwa hali ni mbaya kupita kiasi.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Geert Cappelaere amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani wakati huu ambapo inaelezwa mfumo wa afya Yemen umesambaratika na visa vya ugonjwa wa kipindupindu vimefikia 100,000.

Amesema machungu ya watoto si katika ugonjwa huo tu usababishwa na maji machafu, bali pia utapiamlo uliokithiri au unyafuzi, kiwango kikitajwa kuongezeka maradufu ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.

Bwana Cappelaere amesema watoto wameumia vya kutosha licha ya magonjwa, shuleni hawawezi kwenda akisema kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua na zaidi ya yote kuna matumaini..

(Sauti ya Geert Cappelaere)

"Nimekuwa wazi kabisa kwa pande zote kuhusu kile kinachotakiwa kufanyika ili kuzuia mlipuko zaidi na pia kutibu watoto. Pande zote zimesikia na zimekubali na siku mbili zilizopita nimepata ahadi kutoka Wizara ya mambo ya nje ya serikali inayotambuliwa Yemen kuwa wataazimia kulipa mishahara ya wafanyakazi.”

Ukosefu wa mishahara ni mojawapo ya chanzo cha ukosefu wa huduma za kijamii nchini Yemen kwa kuwa baadhi ya watendaji hawajalipwa mishahara kutokana na mapigano yanayoendelea tangu mwaka 2015.