Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhila kwa raia wanaokimbia machafuko hayahesabiki-Guterres

Madhila kwa raia wanaokimbia machafuko hayahesabiki-Guterres

Licha ya juhudi za kimataifa, raia wanaendelea kubeba gharama za vita kote duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia baraza la usalama Alhamisi. Katika taarifa yake kwenye mjadala wa wazi kuhusu ulinzi wa raia António Guterres amekumbusha kuhusu hadithi mbalimbali za kusikitisha alizozisikia kutoka kwa wanawake, wanaume na wavulana waliokimbia ili kuokoa maisha yao wakati alipokuwa Kamishina mkuu wa wakimbizi.

Amesema madhila wanayopitia hayahesabiki, na kuonya kwamba mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na vifaa yanaendelea. Amelaani hali ya kuwanyima kwa makusudi wahudumu wa misaada fursa ya kuwafikia wahitaji inayotekelezwa na pande kinzani katika mizozo akisema hiyo inawafikisha watu katika hali isiyovumilika hasa wanapokosa chakula na huduma za afya katika maeneo yanayozingira akitolea mfano Aleppo, Syria,  Juba nchini Sudan Kusini na Mosul nchini Iraq.

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.(Picha:UM/Eskinder Debebe)
Amesema maeneo hayo yamegeuka kuwa mitego ya vifo kwani hata hospitali na shule havisalimiki

(SAUTI YA GUTERRES)

“Mashambulizi katika hospitali, wahudumu wa afya na uporaji wa misaada kutoka katika misafara ya kibinadamu ni dalili ya kuendelea kwa upuuzaji wa sheria za kimataifa na ulinzi wa raia. Ukaliti wa kingono ikiwemo ubakaji utekaji,usafirishaji haramu wa watu, utumwa wa ngono na ndoa za lazima vinachangia katika madhila kwa wanawake na wasichana katika vita.Wanawake wako hatarini zaidi katika matatizo ya mijini kunapozuka misako na operesheni kwenye makazi ya watu na vituo vya ukaguzi. Ukatili huu umewalazimisha mamilioni ya raia kukimbia kwenda kusaka usalama.”

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 65 wametawanywa na machafuko, ghasia na mauaji kote duniani huku theluthi mbili kati yao wakiwa wakimbizi wa ndani katika nchi zao.

Katibu Mkuu ametaja baadhi ya hatua za kuchukua ili kupunguza madhila kwa raia vitani ikiwemo kutoa msaada zaidi kwa mahakama za kimataifa, kutoa kipaumbele katika ulinzi wa raia kwenye operesheni za amani za Umoja wa Mataifa, kuwalinda wakimbizi na kukabiliana na mizizi ya watu kutawanywa.