Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kismaayo yapata kituo cha kujenga stadi za vijana

Kismaayo yapata kituo cha kujenga stadi za vijana

Hii leo huko Kismaayo ambao ni mji mkuu wa muda wa jimbo la Jubaland nchini Somalia, kimefunguliwa rasmi kituo cha kusaidia kuwajumuisha kwenye jamii, DDR, wapiganaji wa zamani wa kikundi cha kigaidi cha Al –Shabaab.

Kituo hicho ni cha nne kufunguliwa nchini humo kama sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuwapatia tiba na kuwalea wapiganaji hao wa zamani.

Ujenzi wake unatokana na ushirikiano kati ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, serikali ya Ujerumani, serikali kuu ya Somalia, serikali ya jimbo la Jubaland na wadau wa maendeleo.

Staffan Tillander ni mkurugenzi wa utawala wa sheria na usalama, UNSOM

(Sauti ya Staffan)

“Hii ndiyo njia ya kuwezesha maendeleo. Bila amani, hakutakuwepo na maendeleo na kituo hiki kitasaidia kuepusha misimamo mikali. Itakuwa na mipango mipana zaidi ya usaidizi ikiungwa mkono na Ujerumani, Japan na wengineo na ushauri utapatia vijana fursa mbadala za ajira, elimu na pia maendeleo ya jamii.”

Kwa upande wake serikali ya Somalia imeshauri vijana kutumia vyema muda wao katika kituo hicho ikieleza kuwa asilimia 75 ya raia wa nchi hiyo ni vijana hivyo itakuwa ni bahati mbaya sana iwapo watashindwa kutumia vema fursa katika kituo hicho.

Uzinduzi ulipambwa na matukio mbalimbali ikiwemo gwaride kutoka kikosi cha muungano wa Afrika huko Somalia, AMISOM.