Hali ya Mosul yazidi kutwamisha maisha ya raia- UM

Hali ya Mosul yazidi kutwamisha maisha ya raia- UM

Nchini Iraq, mapigano katika mji wa Mosul yamezidi kutwamisha hali ya kibinadamu na hivyo mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamechukua hatua kusaidia hali hiyo ikiwemo usaidizi wa chakula na pia kisheria.

Mathalani shirika la mpango wa chakula la umoja huo, limesema hali ya chakula ni mbaya magharibi mwa Mosul ambako wakazi 750,000 wanaishi kihohehahe.

WFP inasema ingawa ni vigumu kuingia maeneo ya ndani kupata taarifa sahihi, wadau waliozungumza na baadhi ya familia kwa njia ya simu wameelezwa kuwa bei ya chakula iko juu na mapigano yanasababisha watu hata waogope kutoka nje kusaka chakula hicho.

Dina El-Kassaby ni msemaji wa WFP,huko Cairo Misri anasema sasa wanalazimika kuwapatia msaada..

(Sauti ya Dina)

“Tunawapatia mlo kama vile mgao wa vyakula muhimu ikiwemo biskuti zenye virutubisho. Na ni vyeme kuwa vyakula hivi havihitaji kupikwa. Hadi sasa tumesaidia watu elfu sita waliokimbia magharibi mwa Mosul.”

Nayo UNHCR ambayo inajikita na wakimbizi imechukua hatua kuwapatia vitambulisho au nyaraka muhimu raia zaidi ya 2,500 ambao walipoteza nyaraka hizo wakati wakikimbia kuokoa maisha yao.

Nyaraka hizo kama vile vyeti za kuzaliwa na vile vya ndoa, ni miongoni mwa nyaraka muhimu za kuwawezesha raia kupata huduma kama vile makazi na pia kusafiri.