Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la msongo wa mawazo laonyesha pengo kubwa katika tiba: WHO

Ongezeko la msongo wa mawazo laonyesha pengo kubwa katika tiba: WHO

Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa la afya ya akili kuliko wengi wanavyodhani, na idadi ya wagonjwa inaongezeka kwa mujibu wa taarifa ya wataalamu wa afya wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Alhamisi.

Katika harakati za kuelimisha umma kuhusu tatizo hilo Shirika la afya ulimwenguni, WHO imetangaza kwamba zaidi ya watu milioni 300 hivi saaa wanaishi na msongo wa mawazo kote duniani ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 kati ya mwaka 2005 na 2015.

Shirika hilo linasema nchi masikini ndio waathirika wakubwa,wakiwa na msaada mdogo au hakuna kabisa kwa watu wanaohitaji huduma. Takwimu mpya zinaonyesha kwamba zaidi ya mtu mmoja kati ya 25 wana msongo wa mawazo na ugonjwa huo upo zaidi miongoni mwa wanawake kuliko wanaume na umekuwa moja ya maradhi yanayoongoza kwa kusababisha ulemavu duniani.

Hata hivyo hatua ndogo sana zinachukuliwa kushughulikia tatizo hilo. Dr Dan Chisholm wa WHO anaongoza kampeni dhidi ya msongo wa mawazo ijulikanayo kama “Depression: Let’s Talk”

(SAUTI YA DR DAN CHISHOLM)

“Ni tatizo kubwa ,na ni kwa sababu ya pengo la matibabu ukilinganisha , idadi ya watu wanaohitaji huduma na wanaopata ni ndogo sana katika nchi za kipato cha chini na cha wastani , ni kama asilimia tano tu hivyo kuna pengo la asilimia 95 la matibabu kwa watu wenye ugonjwa huu na hiyo ni hofu kubwa”

Msongo wa mawazo huathiri watu wa rika zote , wa aina zote za maisha nan chi zote. Kwa mwaka 2015 WHO inasema umeshilikia nafasi ya pili kwa kusababisha vifo miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 29, ukikatili jumla ya maisha ya watu 800,000 wengi ikiwa ni kwa kujiua.