Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaunga mkono mapendekezo ya kodi kwa vinywaji vya sukari Afrika Kusini

WHO yaunga mkono mapendekezo ya kodi kwa vinywaji vya sukari Afrika Kusini

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema linaunga mkono mapendekezo ya serikali ya Afrika Kusini kutaka kuanzisha utozaji wa kodi kwa vinywaji vyenye sukari (SSB) ili kupunguza matumizi makubwa ya sukari.

Hatua hiyo ni moja ya njia ziliopendekezwa katika mikakati ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti utipwatipwa nchini Afrika Kusini kwa mwaka 2015-2020.

WHO imeunga mkono uanzishwaji wa kodi hiyo tangu ilipopendekezwa na ofisi ya hazina ya kitaifa mwezi Agosti 2016.

Mwakilishi wa WHO nchini Afrika Kusini, Dr Rufaro Chatora, alishiriki mjadala wa bunge uliofanyika Januari 31 kujadili mapendekezo hayo na kuainisha ushahidi na faida za kutoza kodi vinywaji vyenye sukari kwa afya ya umma ikiwemo kudhibiti kisukari, utipwatipwa na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza (NCDs).