Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mtikisiko kwenye bei za vyakula- FAO

Hakuna mtikisiko kwenye bei za vyakula- FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema bei za vyakula vinavyotegemewa zaidi zilipungua kwa mwaka wa tano mfululizo mwaka 2016.

Taarifa ya FAO imesema kipimo cha bei za vyakula hivyo kama vile nafaka, mafuta, nyama, sukari na bidhaa za maziwa zilipungua kwa zaidi ya pointi 161.1 mwaka jana ikiwa ni pungufu kwa asilimia 1.5 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia wa 2015.

Hali hiyo ilidhihirishwa na bei za vyakula kutobadilika mwezi Disemba mwaka jana ikilinganishwa na mwezi Novemba.

FAO imetaja sababu za kushuka kwa bei kuwa ni pamoja na kiwango kikubwa cha uzalishaji wa ngano kuliko ilivyotarajiwa huko Australia, Canada na Urusi.

Mchumi mwandamizi wa FAO Abdolreza Abbassian amesema wasiwasi wa hali ya kiuchumi ikiwemo mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha vinaweza kuathiri zaidi masoko ya chakula kwa mwaka huu wa 2017.