Idadi ya wahitaji wa maji Damascus yafikia milioni 5.5

Idadi ya wahitaji wa maji Damascus yafikia milioni 5.5

Nchini Syria takribani watu milioni 5.5 kwenye mji mkuu Damascus, bado wanakabiliwa na uhaba wa maji kufuatia kuharibiwa kwa mabomba makuu yanayosafirisha maji tangu tarehe 22 mwezi uliopita.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa majanga, OCHA imesema kufuatia hali hiyo ina hofu kubwa ya mlipuko wa magonjwa yanayoenezwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama hususan miongoni mwa watoto.

Eneo lililoathiriwa zaidi ni Wadi Barada ambapo OCHA inasema tayari mamlaka za maji zimechukua hatua angalau kukidhi mahitaji kidogo ya maji.

Mathalani mjini Damascus magari yanatumika kusambaza maji kwenye shule, hospitali, maduka ya kuoka mikate na kwenye viunga vingine.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake umekarabati visima pamoja na kusambaza mafuta na jenereta kusaidia kusukuma maji kutoka visimani.