Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi wa Gambia; Zeid aonya ukiukwaji wa haki za binadamu

Uchaguzi wa Gambia; Zeid aonya ukiukwaji wa haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al Hussein amesema kuendelea kutawanywa kwa vikosi vya jeshi kwenye maeneo mbali mbali nchini Gambia tangu Rais Yahya Jammeh akatae matokeo ya uchaguzi wa rais kunaweza kuleta hatari na vitisho nchini humo. Rosemary Musumba na ripoti kamili.

(Taarifa ya Rosemary)

Zeid katika taarifa yake amesema kinachoendelea sasa kinatia hofu kwa kuzingatia rekodi ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Gambia ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji, watu kuwekwa kizuizini kiholela na vifo na madai ya mateso na ukatili dhidi ya wafungwa.

Amekumbusha serikali kuwa raia wana haki ya kufanya mikutano kwa amani na wana uhuru wa kukusanyika na kujieleza. Kamishna Zeid ametaka wale wanaohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu wawajibishwe.

Ameziomba pande zote za kisiasa kuthibitisha dhamira yao ya demokrasia na kufanya kazi kuhakikisha kuwa kuna makabidhiano ya amani ya urais tarehe 18 mwezi ujao kwa kuzingatia matakwa ya watu wa Gambia.

Rais Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 22, awali alikubali ushindi wa mpinzani wake Adama Barrow lakini baadaye alikataa matokeo yaliyochapishwa na Tume huru ya uchaguzi akidai kuna ukiukaji wa kanuni.