Dola milioni 241 zaombwa kusaidia wakimbizi bonde la ziwa Chad
Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amezindua ombi la dola milioni 241 ili kusaidia zaidi ya watu nusu milioni waliokwana huko Niger, Chad na Cameroon kutokana na mashambulizi ya Boko Haram kwa mwaka ujao wa 2017.
Uzinduzi huo umefanyika huko Yaounde Cameroon ambako fedha hizo zinalenga kusaidia pia zaidi ya wakimbizi 183, 000 kutoka Nigeria.
Bwana Grandi amesema eneo hilo la bonde la ziwa Chad lina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi barani Afrika na kwamba dunia haipaswi kufumbia macho akisema ameshuhudia machungu makubwa wanayopitia wakimbizi hao.
Halikadhalika Kamishna huyo mkuu wa UNHCR ameahidi kuchagiza mashirika ya maendeleo kuwekeza miradi kwenye ukanda huo ili janga linaloendelea liweze kushughulikiwa kwa ubunifu na ugunduzi.
Ombi lililozinduliwa leo ni nyongeza ya dola milioni 43 ikilinganishwa na ombi la mwaka huu wa 2016 ambalo hata hivyo limechangiwa kwa asilimia 43 tu.