Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa Paris waanza kutekelezwa leo

Mkataba wa Paris waanza kutekelezwa leo

Hatimaye mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi unaanza kutekelezwa leo tarehe 4 ya mwezi Novemba.

Hii ni baada ya kutimia na hata kuvuka kiwango cha idadi ya nchi zinazotakiwa kuridhia ili uanze kutekelezwa.

Mkataba huo ambao unalenga kupunguza ongezeko la joto duniani ili kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ulihitaji nchi 55 zinazochangia asilimia 55 ya gesi chafuzi zitie saini na kuridhia mkataba huo uliopitishwa mwezi Disemba mwaka jana huko Paris, Ufaransa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akizungumzia kuanza kutekelezwa kwa mkataba huo amesema ni siku ya kihistoria kwa binadamu na sayari kwa kuwa kila nchi imekubali kudhibiti ongezeko la kiwango cha joto duniani.

Amesema kila taifa limeahidi kujenga uwezo wa kukabili mabadiliko yajayo kwa njia mbali mbali ikiwemo kwa kutumia nishati mbadala na endelevu.

Hata hivyo amesema hatua zaidi zahitajika kutoka sekta zote za umma na zile za kibinafsi, makundi ya kidini, vijana na raia popote walipo ili kuwa na dunia bora kwa wote.

Hatua ya leo inaendana sanjari na shughuli mbali mbali duniani ambapo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Ban Ki-moon ataongoza tukio rasmi la uzinduzi wa utekelezaji wa mkataba huo.

Mkutano huo utakuwa mbashara kwenye televisheni ya mtandaoni ya Umoja wa Mataifa