Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu watawanywa na machafuko mapya Sudan Kusini- UNHCR

Maelfu watawanywa na machafuko mapya Sudan Kusini- UNHCR

Mgogoro wa Sudan Kusini ambao umesababisha moja ya zahma kubwa ya kibindamu, unaendelea kuleta madhila na kuwatawanya maelfu ya watu.

Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, takwimu za mwezi Oktoba zinaonyesha kwamba kwa wastani kila siku watu 3,500 wanakimbilia nchi jirani za Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia na Sudan.

Katika nchi hizo UNHCR, uongozi wa kitaifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wanakimbizana kuweka mazingira salama na ya kibinadamu kwa watu wanaowasilina ambao tisa kati ya 10 ni wanawake na watoto.

Uganda ndio inayopokea mzigo mkubwa takribani watu 2400 kila siku tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba, na imeshapokea zaidi ya wakimbizi robo milioni tangu kuzuka kwa machafuko mapya.