Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya SEED 2016 ni pamoja na magugu maji yanayotengeneza mbolea asili

Tuzo ya SEED 2016 ni pamoja na magugu maji yanayotengeneza mbolea asili

Kampuni 20 zinazotumia mbinu bunifu za kubadili takataka kuwa bidhaa au huduma bora zimeibuka washindi wa tuzo ya mwaka huu 2016 ya bidhaa zinazojali mazingira, au SEED.

Shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP limesema kampuni hizo ni pamoja na ile ya watu wenye ulemavu kutoka Ghana ambao wanatengeneza viatu kwa kutumia tairi zilizochoka, nyingine ni ya Kenya inayotumia plastiki chafu kutengeneza barabara, bila kusahau kampuni ya Burkina Faso inayotengeneza mbolea asili kutokana na magugu maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Erik Solheim amesema ushindi wa kampuni hizo ni dhihirisho jinsi kampuni ndogo zinavyochangia kuchochoea uchumi unaojali mazingira katika nchi zinazoendelea.

Amesema washindi hao ni mifano wa kipekee wa jinsi vipaji vya ujasiriamali vinayosaidia siyo tu kufanikisha malengo ya kujali mazingira, bali pia kuwa chachu kwa watu binafsi na kampuni katika kufanikisha lengo hilo.

Washindi wa tuzo ya SEED iliyoanzishwa na UNEP mwaka 2002, wanapatiwa tuzo zao leo huko Nairobi, Kenya ambapo pia watapatiwa usaidizi wa kiufundi kwa miezi sita ili kuboresha bidhaa zao.