Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uamuzi wa mahakama ukisubiriwa Gabon, Ban ataka utulivu

Uamuzi wa mahakama ukisubiriwa Gabon, Ban ataka utulivu

Viongozi wa kisiasa na wafuasi wao nchini Gabon wameaswa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon kujizuia na kudumisha utulivu , wakati taifa hilo likisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu uchaguzi wa Rais uliofanyika hivi karibuni.

Mahakama ya katiba ya nchi hiyo itatoa uamuzi wake leo Ijumaa kuhusu mzozo wa matokeo ya kura baina ya rais wa sasa Ali Bongo na mgombea wa upinzani Jean Ping.

AKatibu mkuu ameutaka uongozi wa nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi kuheshimu haki za binadamu na uhuru mwingine katika kipindi hiki cha changamoto na kujiepusha na ghasia za aina yoyote ile.

Wananchi wa Gabon walipiga kura Agosti 27 na matokeo ya awali yaliyotolewa siku chache baadaye yameonyesha Rais Ali Bongo ameshinda kwa takribani kura 6000. Baada ya kutangazwa matokeo hayo ghasia zililipuka mji mkuu Libreville, na Ban amesema uongozi una wajibu wa kuhakikisha ghasia kama hizo hazitokei tena.