Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka serikali ziboreshe upatikanaji elimu kwa watu wa asili

Ban ataka serikali ziboreshe upatikanaji elimu kwa watu wa asili

Katika kuadhimisha siku ya watu wa asili Agosti Tisa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amezitaka serikali ziboreshe upatikanaji wa elimu kwa watu wa jamii za asili, pamoja na kujumuisha uzoefu na utamaduni wao kunakotolewa elimu.

Ban amesema msingi wa Ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu ni kutomwacha mtu yeyote nyuma katika safari ya kufikia ulimwengu wenye amani na hadhi, fursa, na ufanisi.

Katibu Mkuu amesema miongoni mwa walio katika hatari ya kuachwa nyuma ni watu wa jamii za asili, ambao hukabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo ubaguzi wa kimfumo, kunyimwa haki za ardhi na mipaka yao, pamoja na kutowezeshwa kupata huduma muhimu.

Ban amesema haikubaliki kwamba kote duniani, kiwango cha vijana wanaofuzu elimu ya sekondari kutoka jamii za asili ni chini ya wastani wa kitaifa, huku katika baadhi ya nchi, watoto wa jamii za asili wanaokwenda shule ipasavyo wakiwa chini ya asilimia 40.