Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Syria wajiandae na likizo ya kiangazi sio kuhepa mabomu: UNICEF

Watoto Syria wajiandae na likizo ya kiangazi sio kuhepa mabomu: UNICEF

Watoto walioko katika maeneo yenye mizozo nao wajiandae kwa ajili ya majira ya kiangazi kama walivyo watoto wengine ambao hufurahia kipindi hicho cha hali nzuri ya hewa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNICEF.

UNICEF katika taarifa yake ikimnukuu mwakilishi wake nchini Syria Hanaa Singer imesema mtoto mmoja ameuawa na makumi wengine kujeruhiwa kufuatia kulipuliwa kwa mabomu mjini Damscus jana huku takribani watoto watano wakiripotiwa kuawa kufuatia shambulio katika soko la Idlib hii leo.

Bi Singer amesema taarifa hizi zinakuja wakati huu ambapo kumekuwa na matukio ya mashmbulizi kwa raia katika majuma yaliyopita ambapo makumi ya watoto wameripotiwa kuawa na kuongeza kuwa watoto nchini Syria wamekuwa wakisimulia mikasa ya kutisha.

Akisisitiza wito wake ameeleza kuwa badala ya kuhepa mabomu na risasi watoto wanapaswa kujiandaa na likizo ya majira ya kiangazi na kwamba wengi wao wamepitia madhila kiasi kwamba hawawezi kulala na hata wanaolala hukumbwa na majinamizi na wengine hawawezi kuongea tena.