#WHS: Ushirika wazinduliwa kusaidia nchi kuhimili majanga
Ushirika mpya wa kimataifa wa kuwezesha nchi kujiandaa majanga, GPP, umezinduliwa leo huko Istanbul, Uturuki ukihusisha mataifa 43 yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, na mashrika ya Umoja wa Mataifa, wakati huu ambapo dharura za kibinadamu zinaongezeka kila uchao.
Roberto Tan, kutoka Ufilipino ambaye ni mwenyekiti wa mataifa hayo, amesema lengo la ubia huo ni kuhakikisha majanga yanapotokea, mifumo ya usaidizi iko tayari kusaidia jamii ili ziweze kurejea katika maisha ya kawaida haraka iwezekanavyo.
Wadau ni pamojana shirika la mpango wa chakula duniani, WFP ambalo Mkurugenzi Mtendaji wake Ertharin Cousin amesema ushirika huo utaanza kazi baadaye mwaka huu ukianza na nchi 20 zitakazopatiwa mifumo ya kupata taarifa za onyo dhidi ya majanga, mipango dhahiri ya usaidizi na hatua za kuchukua pamoja na mifumo ya usaidizi wa kijamii.
Naye Kiongozi mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, Helen Clark amesema nchi nufaika siyo tu zitaweza kuhimili na kuibuka bali pia zitaweza kulinda mafanikio yaliyopo ili yasipotee majanga yanapotokea.
Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa ni pamoja na OCHA, Benki ya Dunia na FAO.