Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#WHS yaridhia hati ya kulinda maslahi ya watu wenye ulemavu

#WHS yaridhia hati ya kulinda maslahi ya watu wenye ulemavu

Pamoja na mambo mengine hati hiyo inasihi serikali na mashirika ya kiraia sambamba na wahisani kuhakikisha hatua zote za kibinadamu wakati wa majanga zinakidhi misingi mitano.

Misingi hiyo ni pamoja na kutobagua na kutambua aina mbali mbali za ulemavu wakati wa majanga, kushirikisha watu wenye ulemavu katika mipango ya usaidizi wa kibinadamu, kuhakikisha mipango yote ya usaidizi inafikishiwa watu wote wenye ulemavu na kutekeleza sera shirikishi.

Akizungumzia hatua hiyo, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu Catarina Devandas-Aguilar amesema ujumuishaji wa hatua dhidi ya majanga ya kibinadamu na watu wenye ulemavu ni jambo thabiti.

Amesema mara nyingi wakati wa majanga watu wenye ulemavu husahaulika na hatua za kuwasaidia zinakuwa ni ngumu kutokana na ukosefu wa mipango ya awali.

Mtaalamu huyo amesema hali hiyo ni dhahiri mara nyingi wakati wa vita na majanga asilia.