Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#WHS yafunga pazia, wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama wakwepa

#WHS yafunga pazia, wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama wakwepa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekosoa kitendo cha wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokushiriki mkutano wa utu wa kibinadamu  uliomalizika leo huko Istanbul, Uturuki.

Akizungumza na wanahabari, kwenye mkutano uliohudhuriwa pia na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Katibu Mkuu amesema…

 “Mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa baraza la usalama umezuia maendeleo miaka ya karibuni siyo tu kwenye masuala nyeti kama vita na amani bali pia yale ya kibinadamu. Na ndio maana nawasihi viongozi wa nchi zenye ujumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama wachukue hatua za kiwango cha juu. Kutokuwepo kwenye mkutano huu si kisingizio cha kutochukua hatua.”

Ban akaenda mbali zaidi akisema..

“Inakatisha tamaa kuwa baadhi ya vinogozi hasa wale wa nchi zilizo mbele kiuchumi zaidi duniani, G7 hazikushiriki, isipokuwa Ujerumani ambayo imewakilishwa na Kansela Angela Merkel. Hizi ni baadhi ya nchi karimu zaidi katika masuala ya ubinadamu. Lakini  naomba ushiriki zaidi hasa kwenye kusaka suluhu za kisiasa.”

Licha ya kutokuwepo kwa viongozi hao, Ban akizungumza kwenye hafla ya kufunga mkutano huo amesema umekuwa na mafanikio kwani serikali, watu walioathiriwa na majanga, mashirika ya kiraia na  yale ya Umoja wa Mataifa pamoja na sekta binafsi wameunga mkono ajenda ya utu wa kibinadamu na misingi yake mikuu mitano.

Hivyo amesema mwezi Septemba mwaka huu atawasilisha matokeo ya mkutano huo kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa.