Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yalaani shambulio la Sortony, yatoa wito wa kujizuia na ghasia

UNAMID yalaani shambulio la Sortony, yatoa wito wa kujizuia na ghasia

Mpango wa pamoja wa Umoja wa mataifa na Muungano wa Afrika kulinda amani Darfur UNAMID, umelaani vikali shambulio lililotokea Jumatatu kwa baadhi ya wakimbizi wa ndani eneo la Sortony, Kaskazini mwa Darfur.

Kwa mujibu wa UNAMID watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari la kujihami na silaha walivyatua risasi na kuua watoto wawili na kujeruhi wengine kadhaa akiwemo mlinda amani wa UNAMID.Na katika harakati za kujihami walinda amani wa UNAMID walifanikiwa kuwakamata watu wawili miongoni mwa wanaodaiwa kutekeleza shambulio hilo na wako katika mchakato wa kuwakabidhi kwa uongozi wa serikali ya Sudan katika eneo la Kabkabiya.

Awali siku hiyo majibishano ya risasi yalitokea sokoni mita chahe kutoka eneo hilo la wakimbizi wa ndani ambapo watu watatu waliuawa na wanne kujeruhiwa. Majeruhi wanapatiwa matibabu kwenye kliniki ya UNAMID mjini Sortony. UNAMID imetoa wito wa kujizuia na kukomesha mara moja mashambulizi ya aina hiyo.