Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adama Deng apazia sauti hali ya raia nchini Syria

Adama Deng apazia sauti hali ya raia nchini Syria

Mshauri maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, ameeleza kusikitishwa mno na mashambulizi holela na yale yanayowalenga raia na miundombinu ya kiraia moja kwa moja nchini Syria, kufuatia wiki mbili zenye umwagaji damu zaidi tangu makubaliano ya sitisho la mapigano, ambalo lilianza kutekelezwa mnamo Februari 27, 2016.

Taarifa ya Bwana Dieng imesema kati ya Aprili 27 na Mei 5 2016, kulikuwa na angalau mashambulizi sita yaliyofanywa na pande tofauti katika mzozo wa Syria dhidi ya vituo vya afya kaskazini magharibi mwa nchi, katika jimbo la Aleppo pekee.

Shambulizi moja dhidi ya hospitali ya Al Quds mnamo Aprili 27 liliripotiwa kuwaua raia 55, akiwemo daktari wa watoto pekee aliyekuwa amesalia katika mji huo, huku jingine la Mei 5 kaskazini mwa nchi dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani katika jimbo la Idlib likiwaua watu wapatao 30.

Mshauri huyo wa Katibu Mkuu amesema jamii ya kimataifa haiwezi kuruhusu wakiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu kuendelea kufurahia ukwepaji sheria, akikariri azimio la Baraza la Usalama namba 2286 linalozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zitimize wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa na kuhakikisha kuwa pande zote zinawajibishwa.