Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria ya kulinda unyonyeshaji ni hafifu katika nchi nyingi-WHO/UNICEF

Sheria ya kulinda unyonyeshaji ni hafifu katika nchi nyingi-WHO/UNICEF

Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), lile la kuhudumia watoto (UNICEF) na asasi ya mtandao wa kimataifa kuhusu chakula cha watoto (IBFAN), imebainisha kuwa sheria za kulinda unyonyeshaji wa watoto katika nchi nyingi ni hafifu.

Kati ya nchi 194 zilizozingatiwa katika tathmini ya ripoti hiyo, ni nchi 39 tu ndizo zilizo na sheria zinazotimiza kanuni zote za kimataifa na maazimio ya Baraza la Afya Duniani kuhusu matangazo ya biashara kuhusu bidhaa zinazotumiwa badala ya maziwa ya mama.

WHO na UNICEF zinapendekeza kwamba watoto wasilishwe kitu kingine chochote katika miezi sita ya kwanza, ila kunyonyeshwa tu maziwa ya mama, na baada ya miezi sita, waendelee kunyonyeshwa  hadi watakapotimu umri wa miaka miwili, wanapolishwa vyakula vingine vyenye lishe bora

Nchi wanachama wa WHO zimeahidi kuongeza viwango vya unyonyeshaji pekee kwa miezi sita ya kwanza hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2025, ambalo ni moja ya malengo ya lishe.

Kanuni hizo ni wito kwa nchi kulinda unyonyeshaji, kwa kukomesha utangazaji usiofaa wa bidhaa zinazotumiwa badala ya maziwa ya mama, mathalan ‘formula’ na chupa za kuwalishia watoto, na kupiga marufuku uwekaji vibandiko vinavyoongeza umaarufu kwenye bidhaa hizo.